Mnamo tarehe 8 Oktoba, 2014, Rais Uhuru Kenyatta wa jamhuri ya Kenya aliingia katika vitabu vya historia kama rais wa kwanza wa taifa lolote kufika katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, akiwa mamlakani. Rais Kenyatta anatuhumiwa kufanya uhalifu dhidi ya utu, kufuatia mgogoro wa matokeo ya uchaguzi wa urais wa 2007.
Hata hivyo, hali ambayo ingekuwa hatua kubwa katika historia ya mahakama iligubikwa na ukweli kwamba kuanzishwa kwa kesi ya Rais Kenyatta kulikuwa kumeahairishwa mara kadhaa. Alikuwa akidhudhuria kikao cha kutathmini hali ya kesi yake, ili kupata mwelekeo wa mkondo utakaofuatwa. Hii ilikuwa ni kufuatia kauli ya kiongozi wa mashtaka katika mahakama hiyo, aliyekiri kutokuwa na ushahidi wa kutosha kuendeleza kesi hiyo, baada ya vifo au kujiondoa kwa mashahidi muhimu, pamoja na ulegevu wa serikali ya Kenya katika kuwasilisha ushahidi muhimu. Waama, ilitiliwa shaka sana iwapo kesi hiyo ingewahi kuanza. Hata hivyo, kufika kwa Rais Kenyatta mahakamani kunatoa nafasi muhimu ya kukadiria athari ya mahakama hiyo nchini Kenya.
Rais Kenyatta pamoja na Makamu wake William Ruto, walikuwa miongoni mwa Wakenya sita watajika, walioshtakiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, kufuatia kuenea kwa ghasia zilizofuatia mzozo wa uchaguzi wa urais mwaka 2007. Mashtaka dhidi ya washtakiwa wawili, Henry Kosgey na Hussein Ali yalitupiliwa mbali na baraza la kuidhinisha mashtaka. Kiongozi wa mashtaka, Fatou Bensouda, pia alitupilia mbali mashtaka dhidi ya aliyekuwa kiongozi wa utumishi wa umma, Francis Muthaura, akinukuu kuuawa au kujiondoa kwa mashahidi muhimu. Mashtaka ya William Ruto na mshtakiwa mwenzake, mtangazaji Joshua Sang yangali yanaendelea.
Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ilianzisha uchunguzi nchini Kenya mnamo Machi 2010, baada ya Kiongozi wa Mashtaka, Louis Moreno –Ocampo, kuidhinishwa na mahakama kuanzisha uchunguzi. Hii ilikuwa ni baada ya Kenya kushindwa kuanzisha mahakama ya ndani nchini, na kuwafungulia mashtaka wahalifu wa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007. Uchaguzi huo – ambao ulizua mvutano mkali kati ya Rais Mteule Mwai Kibaki na mpinzani wake wa karibu Raila Odinga- ulikuwa wenye ushindani mkubwa zaidi katika historia ya Kenya. Kampeini pia ziliendeshwa katika mazingira ya mgawanyiko mkubwa, huku chama cha Raila Odinga (ODM), kikijikita katika ukosefu wa usawa na kutengwa kwa makabila madogo, na kuunda Muungano wa nguvu dhidi ya chama cha Kibaki (PNU).
Tume ya Uchaguzi ilipomtangaza Kibaki kuwa mshindi wa uchaguzi huo, licha ya Raila kuonekana akichukua ushindi wa mapema, upinzani ulilalamikia mchezo mbaya na kuyapinga matokeo hayo vikali. Ghasia nyingi zilizuka, huku zikiwaacha watu 1,133 katika mauti, zaidi ya watu 600,000 wakifurushwa makwao, na mamia ya wanawake na wanaume wakidhulumiwa kimapenzi, pamoja na mali zao kuharibiwa. Kwa majuma machache mapema mwaka 2008, Kenya ilinusurika vita vya kitaifa vya wenyewe kwa wenyewe, kufuatia kuingilia kati kwa jamii ya kimataifa, hususan kufuatia juhudi za upatanishi za viongozi mashuhuri wa Kiafrika, chini ya wenyekiti wa Kofi Annan.
Mojawapo wa matokeo ya juhudi zao za upatanishi ilikuwa ni mwafaka wa kuundwa kwa tume ya kuchunguza ghasia za baada ya uchaguzi, iliyopendekeza kuanzishwa kwa mahakama maalum iliyojumuisha majaji wa Kenya na wan nchi za kigeni, ili kusikiza kesi dhidi ya wachochezi wa ghasia hizo. Hata Kenya iliposhindwa kuanzisha mahakama hii maalum nchini, ndipo Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ilipoingilia kati na kuanzisha uchunguzi.
Hapo mwanzoni, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ilipata kuungwa mkono na umma, pamoja na wanasiasa. Wabunge walisikika na mirindimo ya “Hatutaki mahakama ya humu nchini, tunataka Mahakama ya Kimataifa ya Jinai”, katika kupinga kuanzishwa kwa mahakama ya ndani nchini, na kuunga mkono kuingiliwa kwa kesi hizo na Makama ya Kimataifa ya Jinai. Hata hivyo, pamoja na kwamba umma wa Kenya uliunga mkono kwa asilimia kubwa shughuli za mahakama ya jinai, hali hii ilidorora punde kiongozi wa mashtaka alipotangaza majina ya Wakenya sita mashuhuri alionuia kufungulia mashtaka. Bunge la taifa likaanzisha mjadala wa kujiuzulu kutokwa kwa Mkataba wa Roma, nayo serikali ikaanzisha kampeini za kimataifa za kuhairishwa kwa kesi hizo za Kenya, bila ufanisi mkubwa.
Reporter#34145/Demoticx (All rights reserved)
Supporters greet Uhuru Kenyatta's return from The Hague with, "a rapturous and well-choreographed welcome."
Kisiasa, ilipobainika katika 2010 ni kina nani waliyokuwa wakilengwa na mahakama hiyo kushtakiwa, viongozi wa kisiasa wakawa na mshimakamano kwa kasi. Uchaguzi wa 2013 ungetumika kama fursa ya kuimarisha matunda yaliyoahidiwa na katiba mpya iliyoidhinishwa 2010. Badala yake, Uhuru Kenyatta na William Ruto – ambao walikuwa katika pande pinzani wakati wa kampeini za uchaguzi wa 2007- waliunda muungano, na kudai kuwa uchaguzi huo ungekuwa ni kura ya maamuzi kuhusu Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, na wakaungana kwa kuwania urais kwa tikiti moja. Ushindi wao ulioponea chupuchupu dhidi ya Raila Odinga ulishikiliwa na Mahakama ya Juu, ila uamuzi huo ukawaacha Wakenya wamegawanyika zaidi.
Kwa miezi kumi na nane tangu Kenyatta na Ruto waingie mamlakani, wafuasi wao wamekuwa wakishambulia vikali taasisi za mashirika ya kijamii zinazounga mkono juhudi za Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, wakiwaita kwa utani “jamii mbovu”, na kuwachukulia kuwa mawakala wa nguvu za kigeni. Muungano unaotawala umeapa kushinikiza kisheria shughuli za mashirika haya ya kijamii, kwa kuwekea mipaka kiwango cha fedha wanazoruhusiwa kupokea kutoka kwa wafadhili wa kigeni. Mwelekeo huu wa kusikitisha unazua hofu kwamba uhuru wa kidemokrasia ambao Wakenya walipigania kwa jino na ukucha unatishiwa na serikali ya Kenyatta.
Athari nyingine hatari ya shughuli za Makama ya Kimataifa ya Jinai ni kwamba mkazo umetolewa kwa wahasiriwa wa ghasia hizo hadi watuhumiwa, kupitia mbinu za vyombo vya habari zinazotumiwa na washukiwa hao kwa manufaa yao wenyewe. Huku Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ikisakama, taratibu nyinginezo za haki kama vile Tume ya Ukweli, Haki na Maridhiano zimetengwa, kwa kuwa haiwezekani kuzungumzia hatima ya wahasiriwa wa ghasia hizo bila kutuhumiwa kuunga mkono mahakama hiyo ya kimataifa.
Kabla ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai kuingilia kesi za Kenya, hakuna mwanasiasa wa hadhi ya juu aliyewahi kufanywa kuwajibika kwa uhalifu wa kisiasa tangu kupata uhuru, pamoja na mauaji, mateso, ufisadi uliokolea.
Kwa upande mwingine, kesi hizo za Mahakama ya Kimataifa ya Jinai zinatoa nafasi muhimu katika kuimarisha utendakazi wa sheria. Mojawapo ya sababu kuu za ghasia za baada ya uchaguzi ni uwezo wa wahalifu kuepuka adhabu nchini Kenya. Kabla ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai kuingilia kesi za Kenya, hakuna mwanasiasa wa hadhi ya juu aliyewahi kufanywa kuwajibika kwa uhalifu wa kisiasa tangu kupata uhuru, pamoja na mauaji, mateso, ufisadi uliokolea, na ghasia za uchaguzi za 1992 na 1997. Kwa mara ya kwanza katika historia yao, Wakenya wameshuhudia namna wanasiasa wenye ushawishi mkubwa wanaweza kushtakiwa kwa tuhuma za uhalifu. Pia, Wakenya wameona mageuzi muhimu ya taasisi kama vile mahakama, sekta ya usalama na ulinzi wa mashahidi, ambazo zilikusudiwa kuishawishi jamii ya kimataifa kuwa Kenya ilikuwa tayari kushtaki uhalifu wa ghasia za baada ya uchaguzi.
Uhuru Kenyatta alipokuwa akirejea kutoka Mahakama ya Kimataifa ya Jinai na kupata mapokezi yaliyoandaliwa kwa taadhima kuu, kesi dhidi yake zilionekana kuning’inia, kufuatia kutishwa kwa mashahidi na kukataa kwa serikali ya Kenya kushirikiana na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai. Pamoja na juhudi hafifu za kuwashtaki watuhumiwa nchini Kenya, yaelekea wahasiriwa watazikwa katika kaburi la sahau. Yamkini, hii ndiyo sababu Mahakama ya Kimataifa ya Jinai lazima ihakikishe- licha ya changamoto zilizoko - kuwa kesi za Kenya zimefuatiliwa na kuhitimishwa kimantiki na kisheria.